Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim
Ajibu na chipukizi anayekua kwa kasi, Yohana Nkomola wamerejesha
matumaini kwenye timu hiyo na kesho Jumamosi huenda wakawepo kwenye
orodha ya kikosi kitakachoivaa St Louis ya Shelisheli.
Yanga itawakaribisha wapinzani wao hao
katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ajibu anarejea uwanjani akitokea kupona
majeraha ya goti aliyoyapata kwenye Ligi Kuu Bara wakati timu hiyo
ilipovaana na Azam FC na Nkomola yeye alipata maumivu ya misuli katika
mchezo wa Ruvu Shooting.
Daktari Mkuu wa Yanga, Edward Bavu,
alisema wachezaji hao wameanza mazoezi magumu ya pamoja na wenzao juzi
Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
Bavu alisema kurejea kwa wachezaji hao
kumeimarisha kikosi chao kutokana na kupunguza idadi ya wachezaji
majeruhi waliokuwa wanaiandama timu hiyo.
“Niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga kuwa,
wachezaji wetu muhimu waliokuwa majeruhi Ajibu na Nkomola wamepona na
jana (juzi Jumatano) walianza mazoezi ya pamoja na wenzao.
“Kwa maana hiyo hivi sasa wapo fiti
kucheza mechi ya kimataifa kama kocha akihitaji kuwatumia, lakini mimi
kama kocha niseme wapo fiti kwa ajili ya kuipambania timu yao ya Yanga.
“Kipa wetu Rostand (Youthe) aliyepata
majeraha ya enka kwenye mechi iliyopita na Lipuli FC naye anaendelea
vizuri na ameanza mazoezi ya binafsi kwa ajili ya kujiweka fiti kabla ya
kuanza mazoezi magumu ya pamoja na wenzake,” alisema Bavu.