Milio ya risasi na milipuko
imesikika katika kituo cha mafunzo ya kijeshi katika mji mkuu wa
Afghanistan, Kabul, taarifa zinasema.
Shambulio hilo limetokea baada ya shambulio lililowaua watu wengi zaidi miaka ya karibuni kusababisha vifo vya watu zaidi ya 100 Jumamosi.
Shambulio hilo la Jumamosi lilitekelezwa kwa kutumia gari la kubebea wagonjwa lililokuwa limejazwa vilipuzi.
Wapiganaji wa Islamic State na Taliban wamekuwa wakitekeleza mashambulio maeneo mbalimbali nchini humo.
Shambulio hilo la Jumamosi lilitekelezwa wiki moja baada ya shambulio jingine katika hoteli moja ya Kabul kuwaua watu 22 - wengi wao raia wa nchi za nje.
Taliban walisema ndio waliotekeleza mashambulio yote mawili.
Taasisi za kijeshi zimekuwa zikishambuliwa mara kwa mara na wanamgambo.
Oktoba 2017, makurutu 15 wa jeshi waliuawa kwenye mlipuko uliotokea nje ya kituo cha mafunzo ya kijeshi cha Marshal Fahim, ambacho hupatikana magharibi mwa Kabul.