
Aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Abdulhalim Humud ameibuka na kusema kuwa uongozi umemchafua kwa kumpa kashfa ya kuwashawishi wake za wachezaji wenzake ili awe nao kwenye mahusiano.
Uongozi wa KMC uliamua kumruhusu Humud kuwa mchezaji huru baada ya yeye mwenyewe kuomba iwe hivyo kutokana na kile kilichoelezwa ni utovu wa nidhamu alioufanya ndani ya klabu ikiwa ni pamoja na kusahau vifaa vya michezo Dar es Salaam wakati timu ilipocheza na Coastal Union pamoja na kuwasumbua wake wa wachezaji wenzake.
"Wameamua kunichafua jambo ambalo sijalipenda kabisa, nimefundishwa kutojipendekeza kwa mwalimu wala kutotoa rushwa hasa kutokana na baadhi ya viongozi kutaka asilimia kumi kwenye mshahara, nikaamua kujitenga pembeni, nina mke mzuri kuliko wachezaji wote pale KMC," alisema.
Kwa upande wa uongozi wa KMC kupitia Ofisa habari Anwar Binde, umesema kuwa Humud anapaswa atambue kuwa uongozi umesimamia kweli kwa kuwa ushahidi upo wa maandishi pamoja na wake ambao walishawishiwa wapo.
"Asitafute huruma kwa sasa, kama anataka haki basi aende mahakamani kwa kuwa ushahidi upo na KMC ni taasisi inayojiendesha kwa utaratibu, masuala ya malipo kumbukumbu zipo za kila mchezaji iwe alilipwa pesa taslimu ama alilipwa benki," alisema