MWENYEKITI wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Tawi la Zanzibar Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said, akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kuhusiana na maadhimishi ya Siku ya Jumuiya ya Madola Duniani, kuadhimisha kwa kufanya Bunge la Vijana Zanzibar, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani
CHAMA cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Tawi la Zanzibar pamoja na Chama cha Wabunge Wanawake wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola wanakusudia kuadhimisha siku ya Jumuiya ya madola.
Maadhimisho hayo yanatariajiwa kufanyika Machi 12 kwa kuandaa Bunge la vijana Zanzibar katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi chukwani mjini Zanzibar
Akizungumza na Waandishi wa habari Mwenyekiti wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Tawi la Zanzibar Simai Mohammed Said amesema jumla ya Vijana 50 wenye umri usiozidi miaka 30 watakashiriki Bunge hilo.
Alifafanua kuwa vijana hao wanatoka katika mabaraza ya vijana ya Unguja na Pemba ambapo wamechaguliwa na sekretarieti ya Baraza kwa kuwashirikina na Wizara yenye dhamana na masuala ya vijana.
Aidha alisema kuwa Bunge hilo pia limezingatia masuala ya jinsia pamoja na vijana wenye mahitaji maalum likiwa na lengo la kuandaa jukwaa maridhawa la kuwandaa vijana kuwa viongozi bora.
Sambamba na hayo Mwenyekiti huyo amesema Baraza la Wawakilishi Zanzibar limekua likiandaa Bunge la Vijana tokea mwaka 2013 ili kujenga hoja kujadili kwa nidhamu kushirikiana ,kufahamau na kufuata taratibu za kibunge.
Hata hivyo alisema kuwa Bunge la vijana ni muendelezo wa azimio la chama cha mabunge ambapo lina lengo la kuwajengea uwezo wa kujenga hoja kulinda na kuitetea hoja ambayo wanayoijengea.
Vilevile alisema kuwa Bunge hilo linatarajiwa kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na demokrasia ya kibunge,utawala bora pamoja na masuala mengine ambayo yanayokwenda sambamba na siku ya jumuiya ya madola.
Pia alisema kuwa katika bunge hilo wanatarajia kupata maazimio ambayo baadae yatapelekwa katika Baraza la Wawakilishi kupitia kamati ya Maendeleo ya wanawake,Habari na utalii na kuwajengea vijana moyo wa kizalendo kushirikiana kwa stadi za uongozi na kujiamini.
Hata hivyo alisema kuwa bunge hilo siku ya Jumatatu ambayo itakuwa siku ya kilele na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mgeni Hassan Juma anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na ujumbe wa mwaka huu ni kuelekea hatma ya pamoja.