Marubani wawili wamefariki Dunia
katika ajali ya ndege wakati wa kurusha ndege baada ya matengezo katika
Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani karume.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo
lililotekea majira ya saa saba Mchana Uwanjani hapo Muhandisi Mkuu
kutoka kampuni ya Tropical Air David Kisusi amesema ndege hiyo
imeanguka na kuungua na kusababisha vifo kwa marubani hao ambao walikuwa
ndani ya ndege hiyo.
Amesema ndege hiyo yenye usajili wa 5H-TDF
yenye uwezo wa kubeba abiria wanne ni mali ya Chuo cha Usafirishaji cha
Dar-es-Salam (NIT) ambayo ilikuwepo Zanzibar kwa ajili ya matengenezo.
Amesema takriban miezi sita ndege hiyo ipo
hapa Zanzibar kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo ili iweze kutumika
katika chuo cha Usafirishaji .
Daktari Bingwa wa Uchunguzi katika Hospital
ya Kuu ya Mnazi mmoja Msafiri Marijani amethibitisha kutokea kwa vifo
hivyo na amesema vifo hivyo vimesababishwa na kukosa hewa safi wakati wa
ajali hiyo pamoja na kathirika na moto uliotokea wakati wa kuanguka
ndege hiyo.
Amesema uchunguzi ulifanywa katika miili ya
maiti hao mnamo majira ya saa 12:45 jioni pia ulitokana na kukosa
msaada wa kwa muda mrefu tangu ndege hiyo ianguke na kuripuka.
Wakati huohuo mkuu wa Chuo cha usafirishaji
wa anga kutoka Dar es Salaam Dkt. Bwire Rufunjo alifika Zanzibar kwa
ajili ya kufuatilia taarifa za ajali hiyo na amesema wamepokea taarifa
hiyo kwa mshtuko mkubwa kutokana na vifo vya wafanyakazi hao muhimu
katika sekta ya anga.
Aliwataja marehemu kuwa ni Injinia Edger
Alfred Mcha mwenye Umri wa miaka 26 na mwengine ni Dominic Bomani mwenye
umri wa miaka 64 ambao walikuwa wanafanya kazi katika chuo hicho kwa
ufanisi mkubwa.
Aidha amewataka wanafamilia wa Marehemu hao
kuwa wavumilivu katika kipindi hichi kigumu kufuatia msiba huo pamoja
na kutowa wito kwa wanafunzi wa chuo hicho kutokata tamaa wakati wa
masomo.
Akizungumzia sababu ya kuanguka kwa ndege
hiyo ndogo amesema uchunguzi bado unaendelea lakini katika uchunguzi wa
awali ni hitilafu Mfumo wa umeme ambao umesababishwa na moto uliripuka
kutokana na ndege kuwa na Mafuta mengi.
Ndege hiyo imenunuliwa kutoka kampuni ya
Tropical Air ya Zanzibar kwa ajili ya kufundishia Urubani katika Chuo
cha Usafirishaji lakini kutokana na kutokuwa na hali Nzuri ililazimika
kufanyiwa matengenezo na kampuni hiyo kabla kuchukuliwa na chuo.