Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Rugambwa Bwanakunu (kulia), na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Asha Ally Abdullah wakisaini hati ya
makubaliano ya ushirikiano mjini Zanzibar leo. Wengine wanaoshuhudia ni
wanasheria wa taasisi hizo mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Rugambwa Bwanakunu, akielezea namna MSD ilivyojipanga kwenye majukumu yake.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Rugambwa Bwanakunu, akimkabidhi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Asha Ally Abdullah , mpango mkakati wa MSD, 2017-2020, ripoti ya maboresho ya MSD na kitini cha bei za bidhaa za MSD (MSD price catalogue)
Kabla ya kusaini makubaliano hayo Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Rugambwa Bwanakunu (kulia) na timu yake walitembelea ghala la kuhifadhi dawa la Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar (CMS)
Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Afya ya Zanzibar na Bohari ya
Dawa (MSD) wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa MSD kuipatia wizara
hiyo huduma ya kuwasambazia dawa,vifaa tiba na vitendanishi vya maabara
kupitia Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar (CMS)
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuhakikisha wananchi wake wanapata
dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Asha Abdulla amesema changamoto ya
upatikanaji wa dawa ilikuwa kubwa, zikipatikana kwa gharama ya juu na
kiwango kidogo walichohitaji ilikuwa inaleta shida wanapoagiza wenyewe.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni muungano
shairi,na kuipongeza Bohari ya Dawa (MSD) na Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar
(CMS) kwa kutekeleza taratibu zote kwa haraka hadi kufika kusaini
makubaliano hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Bohari ya Dawa (MSD) Laurean Rugambwa Bwanakunu amewahakikishia kuwa
watawapa huduma nzuri,zenye viwango na kwa wakati na bei nafuu kutokana
na kushuka kwa bei ya dawa kwani wananunua dawa moja kwa moja kutoka kwa
wazalishaji.
Ameongeza kuwa pamoja na maboresho ya
kiutendaji yanayoendelea kufanyika MSD,taasisi hiyo pia imeteuliwa kuwa
mnunuzi Mkuu wa dawa,vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa Jumuiya
ya nchi za Ukanda wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hivyo huduma
zake zinakubalika kimataifa,hasa katika mnyororo mzima wa ugavi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa CMS Zanzibar ,
Zahran Ali amesema licha ya makubaliano yaliyofikiwa na kusainiwa,
wamekuwa wakishirikiana na MSD kwa huduma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na
kutoa watalaam wa kuwasaidia kuboresha mnyororo wa ugavi na masuala ya
maoteo sahihi ya mahitaji ya wateja.